Msimamizi wa Adidas amsifia Kanye hata baada ya kusitisha mkataba naye

Marion Bosire
2 Min Read
Ye (Kanye West)

Msimamizi wa sasa wa kampuni ya Adidas Bjorn Gulden amemlimbikizia sifa mwanamuziki Kanye West ambaye alibadili jina na kujiita “Ye” katika hatua inayoshangaza wengi.

Gulden ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo inayounda na kuuza viatu na mavazi ya michezo alikuwa akihojiwa kwenye kipindi fulani cha mitandaoni ambapo alisema kwamba anahisi Ye ni mtu mzuri.

Kulingana naye, Ye hakukusudia kughadhabisha umma kwa matamshi yake kuhusu wayahudi na kwamba yalichukuliwa visivyo.

Alipoulizwa ni kwa nini Adidas ilisitisha mkataba wake na mwimbaji huyo, afisa huyo alisema kwamba Ye alitoa matamshi ambayo hayakuwa mazuri.

Lakini hata hivyo, Bjorn Gulden hakuwa anasimamia kampuni ya Adidas wakati hatua ya kusitisha mkataba na Ye ilitekelezwa. Aliteuliwa kuongoza kampuni hiyo mwezi mmoja baada ya mkataba na Kanye kusitishwa.

Anashikilia kwamba Ye ni mmoja wa wasanii walio na talanta katika ubunifu. Viatu vya Yeezy ambavyo Ye alikuwa anaunda kwa ushirikiano na Adidas Gulden alisema vilikuwa na kiwango cha juu cha mauzo.

Robo ya kwanza ya mwaka huu anasema kampuni hiyo imepata hasara ya Dola milioni 440 kwa sababu ya kukatiza uundaji wa viatu hivyo.

Mwezi Oktoba maka jana, Ye alitamka maneno ya kuudhi kwa wayahudi katika vikao mbali mbali vya mahojiano huku akipinga mpango wa kutetea wamarekani weusi almaarufu “Black Lives Matter” ilhali yeye ni mweusi.

Aliandaa maonyesho ya mitindo ya mavazi ambapo waonyeshaji wake walivaa nguo zilizokuwa na maandishi ya kutetea wazungu ambayo ni, “White Lives Matter”.

Website |  + posts
Share This Article