Maafisa wa Polisi wamemkamata mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati katika eneo la Mandizini, kaunti ya Bungoma.
Kulingana na Huduma ya Taifa ya Polisi, mshukiwa huyo alikamatwa kwenye operesheni ya kijasusi iliyotekelezwa na maafisa hao.
“Baada ya upekuzi wa kina katika makazi ya mshukiwa huyo, polisi walipata vipande 561 vinavyoshukiwa kuwa vya mihadarati, na bidhaa zingine zilizopakiwa kwenye mifuko ya plastiki zinazoshukiwa kuwa za mihadarati.
Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Bungoma, akisubiri kufikishwa mahakamani, huku mihadarati hiyo ikihifadhiwa na itatumika kama ushahidi kwenye kesi hiyo.
Huduma ya Taifa ya Polisi imewahakikishia wananchi kuwa haitalegeza kamba dhidi ya mihadarati, ikitoa wito kwa umma kushirikiana na asasi za usalama kwa kutoa habari muhimu.