Mshukiwa mkuu wa mauaji ya watu wanne katika kaunti ya Nakuru Ezekiel Kwame Mwangi, amekamatwa na maafisa wa idara ya makosa ya jinai DCI.
Mwangi mwenye umri wa miaka 19, ambaye amekuwa akisakwa na maafisa wa polisi, anadaiwa kuhusika na mauaji na visa vya uhalifu katika kaunti ya Nakuru.
Mnamo Julai 14,2024, mshukiwa huyo anadaiwa kumdhulumu kimapenzi na kumuua Alice Ayuma Blessing mwenye umri wa miaka tano, na kutupa mwili wake katika shamba la mahindi katika eneo la Mwangaza.
Kulingana na Idara ya DCI kupitia mtandao wa X, Mwangi pia anatuhumiwa kumuua Mueni Mwalimu mwenye umri wa miaka 34 mnamo Agosti 7, 2024, katika eneo la Kalyet. Mwangi anadaiwa kumgonga mwalimu kwa kifaa butu na kundunga tumboni.
Siku iliyofuatia Agosti 8, 2024 katika eneo la Mustard Seed, Kiamunyi, katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret, Mwangi anadaiwa kumbaka na kumuua Moraa Mugambi mwenye umri wa miaka 28 kwa kumpiga na rungu kichwani.
Idara ya DCI imesema mshukiwa huyo kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Menengai, akisubiri kufikishwa mahakamani.