Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kiikatili dhidi ya watu watatu wa familia moja katika mtaa wa Eastleigh Jijini Nairobi amekamatwa.
Hashim Dagane Muhumed, mwenye umri wa miaka 24 raia wa Somalia, alitiwa nguvuni katika mtaa wa Kamukunji kufuatia operesheni iliyotekelezwa na maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai, DCI.
Miili ya waathiriwa Dahabo Daud Said, Amina Abdirashid na mtoto wa umri wa miaka 12 Museiba Abdi Mahumed, ilipatikana katika maeneo tofauti ya Kyumvi kaunti ya Machakos, Parklands Jijini Nairobi na Shauri Moyo Jijini Nairobi.
Kulingana na Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, uchunguzi ulibainisha kuwa Muhumed ndiye mmiliki wa gari aina ya Nissan Note, lenye nambari za usajili KDQ 718Y, ambayo ilikuwa katika eneo la mkasa.
Video za kamera fiche za CCTV zilionyesha gari hilo likiwekwa mafuta katika kituo cha Total Energies katika eneo la Athi River na pia katika barabara ya Ikulu usiku wa Oktoba 21 na 22, 2024 kabla ya kuachwa kati ya eneo la jumba la Wakulima na lile la KPCU Jijini Nairobi.
Kulingana na video hizo, dereva wa gari hilo alikuwa raia mwenye asili ya Somalia.