Mshukiwa wa mauaji aliyetoroka katika kituo cha polisi cha Muthaiga Kevin Kang’ethe, amekamatwa kufuatia msako wa siku kadhaa uliotekelezwa na maafisa wa polisi.
Kang’ethe mwenye umri wa miaka 40, alikamatwa Jumanne jioni, katika maficho yake mtaani Embulbul kaunti ya Kajiado, na maafisa kutoka kitengo cha operesheni maalum.
Mshukiwa huyo alitoroka katika kituo cha polisi cha Muthaiga, alikokuwa akizuiliwa huku akisubiri uamuzi ikiwa atarejeshwa Marekani kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya mwanamke anayedaiwa kuwa mpenzi wake Margaret Mbitu.
Mahakama moja Jijini Nairobi, ilitarajiwa kutoa uamuzi siku ya Ijumaa iwapo Kevin ashtakiwe nchini Kenya au apelekwe mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji nchini Marekani, baada ya kudai kuwa aliacha uraia wake wa Marekani mwaka jana.
Kang’ethe, ambaye alikamatwa tarehe 30 mwezi Januari mwaka 2024, ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya Margaret Mbitu, aliyeuawa Massachusetts nchini Marekani tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2023.
Kabla ya kukamatwa kwake, maafisa wa polisi waliwahoji watu kadhaa, akiwemo kakake, binamuye pamoja na maafisa wa polisi waliokuwa zamu Kang’ethe alipotoroka.