Maafisa wa upeleleze wa makosa ya jinai DCI, wamemtia nguvuni mshukiwa mwingine kwenye mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya Wells Fargo Willis Ayieko Onyango.
Kulingana na idara hiyo kupitia mtandao wa X, mshukiwa huyo Fredrick Otieno Omondi, alikamatwa mjini Kisumu na anaaminika kutekeleza jukumu muhimu katika mauaji hayo.
Omondi, ambaye ni mhudumu wa bodaboda, anatuhumiwa kutoa huduma za usafiri kwa Victor Ouma Okoth, hadi katika eneo ambalo Onyango alitekwa nyara.
Victor Ouma Okoth kwa sasa anazuiliwa katika korokoro za polisi, baada ya kuhusishwa katika mauaji hayo, pamoja na wengine ambao wanatafutwa na polisi.
DCI ilisema uchunguzi kuhusu mauaji ya Onyango unaendelea, kuhakikisha wote waliohusika katika mauaji hayo wanachukuliwa hatua.