Mshukiwa mkuu katika sakata ya madini ya Tantalum akamatwa

Tom Mathinji
1 Min Read
Mshukiwa Mkuu katika sakata ya Tantalum ya shilingi milioni 151 akamatwa.

Maafisa wa polisi wa idara ya kubakibiala na makosa ya jinai, DCI wamemkamata mshukiwa mkuu anayedaiwa kupokea shilingi milioni 151 ili  kusafirisha madini aina ya Tantalum hadi nchini China lakini badala yake akasafirisha mchanga.

Ulundu Patrick Lumumba almaarufu Gabriel Kulonda, almaarufu Lumumba Patrick Byarufu, alikamatwa katika barabara ya Harambee jijini Nairobi, baada ya kuhepa mtego wa maafisa wa polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA alipowasili kutoka Uganda.

Mshukiwa huyo anahusishwa katika kesi ambapo mwanamke mmoja raia wa China alipoteza shilingi milioni 151 baada ya kasha moja kati ya matatu yaliyowasili nchini China kugunduliwa kuwa na mchanga badala ya madini aina ya Tantalum.

Uchunguzi ulianzishwa mara moja katika bandari ya Mombasa, ambapo makasha mawili yaligunduliwa kuwa na mchanga na kuzuiliwa na maafisa wa DCI.

Kulingana na maafisa wa DCI, makasha hayo yaliidhinishwa katika mchakato wote wa ukaguzi, huku maafisa wa bandari wanaoshukiwa kufanishika mchakato huo wakitiwa nguvuni ili kuhojiwa zaidi.

Mnamo Januari, 30, 2024, polisi walikuwa wamesimamisha matumizi ya pasipoti yake katika idara ya uhamiaji, lakini alipokamatwa alipatikana akiwa na hati nyingine ya kusafiria ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Makachero kutoka DCI watamfikisha mshukiwa huyo mahakamani leo Ijumaa.

TAGGED:
Share This Article