Parastoo Ahmadi ambaye ni msanii wa muziki wa kike nchini Iran, alikamatwa jana Jumamosi Disemba 14, 2024 katika mkoa wa Mazandaran, kwa kufanya tamasha la mtandaoni bila kuvaa vazi la kujisitiri la Hijab.
Ahmadi aliandaa tamasha alilolipa jina la “Caravansara Concert” kwenye akaunti yake ya mtandao wa You Tube Jumatano ambapo alikaidi sheria kali za kimaadili kwa wanawake nchini humo.
Kulingana na sheria hizo, mwanamke hafai kuonekana hadharani bila hijab na haruhusiwi kutumbuiza.
Wakili wake aitwaye Milad Panahipour alihojiwa na wanahabari jana ambapo alisema kufikia saa sita adhuhuri hakuwa amefahamu hali ya mteja wake.
Vyombo vya habari nchini humo viliripoti pia kwamba wanamuziki wawili washirika wa binti huyo ambao ni Ehsan Birghidar na Sohail Faqih Nasiri walikamatwa.
Amefunguliwa kesi kutokana na hatua yake ya kufanya tamasha hilo akiwa ameachia nywele zake wazi.
Bila kumtaja Ahmadi, vyombo hivyo vya habari vimetangaza kwamba mahakama ya Iran imesema katika taarifa kwamba kundi linaloongozwa na mwimbaji mmoja wa kike litumbuiza hadharani bila kuzingatia viwango vya kisheria na kidini vya nchi hiyo.