Juhudi za kutafuta mwili wa afisa wa kliniki aliyetoweka kutoka hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha ziliishia kwenye mauti baada ya mwili wake uliokuwa umeanza kuoza kupatikana ukiwa umezikwa kwenye kaburi la kina kifupi nyumbani kwake.
Mwili wa Jane Wambui Njoroge uligunduliwa nyumbani kwake katika kijiji cha Raini, siku moja baada ya yaya wake kukamatwa kuhusiana na kutokweka kwa daktari huyo.
Hisia zilitanda wakati maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI walipoufukua mwili huo huku uchunguzi wa awali ukifichua kuwa huenda aliuawa kwa kutumia kifaa butu.
Wambui ambaye ni afisa wa kliniki anayesimama wodi ya watoto kwenye hospitali hiyo alionekana mara ya mwisho Ijumaa wiki iliyopita hospitalini hapo.
Tangu wakati huo, hakujulikana alipo kabla ya familia yake kuripoti kisa hicho kwa polisi.
Kulingana na mumewe John Kimani, mara ya mwisho alizungumza na mkewe Ijumaa wiki jana kabla ya kupigiwa simu siku ya Jumapili kuwa hajulikani aliko.
Kimani anayefanya kazi mjini Kitale alisema aliamrisha raia waliokusanyika nyumbani kwake kuvunja nyumba ili kuangalia ikiwa alikuwa nyumbani.
“Mke wangu amekuwa akiigua saratani na nilipoambiwa hapatikani, nilitoa maagizo kwa waliokuwa uani kuvunja nyumba na hawakumpata,” alisema.
Alielezea kushtuka baada ya kufahamu kuwa yaya wao ambaye wamemsaidia miaka nenda miaka rudi amekamatwa kuhusiana na kutoweka kwake.
“Yaya huyo wakati mmoja alikuwa mpangaji wangu ambaye tulikubali kumsaidia kwani hakuweza kulipa kodi na bado nimepigwa na bumbuwazi kwamba alihusika na mauaji haya.”
OCPD wa Naivasha Antony Keter althibitisha kukamatwa kwa yaya huyo akiongeza kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa makamo, baada ya kuhojiwa, aliwapeleka maafisa wa upelelezi palipokuwa na kaburi.
Aliongeza kuwa maafisa DCI wanawatafuta washukiwa wengine ambao huenda walihusika katika mauaji hayo na uzikaji wa mwili.