Bodi ya dawa na sumu, imeimarisha juhudi zake za kukabiliana na usambazaji haramu wa dawa kwenye maduka ya dawa, katika juhudi za kulinda afya ya umma.
Msako huo uliotekelezwa kwa ushirikiano na polisi, ulianza Jumatatu kaunti ya Nakuru, na unalenga huduma za uwasilishaji vifurushi, waendeshaji pikipiki pamoja na wahudumu wa uchukuzi wa umma, ambao hawana leseni ya kusambaza dawa.
Kulingana na afisa anayesimamia msako huo Julius Kaluai, msako huo unalenga kukabiliana na maduka ya dawa yasiyofuata sheria za humu nchini.
Kaluai alitoa tahadhari kwa wahudumu wa bodaboda na pia magari ya umma yasiyo na leseni ya kusambaza dawa hizo, akisema kwamba wanaosambaza dawa lazima wawe wamefikia viwango vinavyohitajika vya kuendeleza shughuli hizo.
Msako huo unawadia siku chache tu baada ya ukaguzi uliofanywa katika vituo vya afya, unaolenga kuangazia changamoto ibuka katika sekta ya afya.
Kadhalika Kaluai alitoa notisi kwa wanaouza dawa kupitia mitandao ya kijamii, kuhakikisha kuwa biashara yao imesajiliwa kama inavyohitajika.
Bodi hiyo imetoa wito kwa umma kuendelea kuwa waangalifu.