Kaunti ya Homabay imekuwa kaunti ya kwanza nchini kupokea cheti cha kuidhinishwa na EDGE kwa mradi wake wa kijani wa nyumba za bei nafuu.
EDGE ni idhinisho la kimataifa la ujenzi lililoanzishwa na shirika la kimataifa la kifedha IFC, tawi la sekta ya kibinafsi la benki ya dunia.
Gavana wa kaunti ya Homabay Gladys Wanga alipokezwa cheti cha mwanzo cha EDGE leo kwenye hafla fupi iliyoandaliwa katika bustani ya Gavana huko Homabay.
Mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu wa Homabay utakuwa na nyumba 400 kwenye ardhi ya ekari 11 mjini Homabay na ndio wa kwanza nchini kati ya miradi yote ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu nchini kupokea idhinisho la EDGE.
Awamu ya kwanza ya mradi huo itakuwa na nyumba 30 za chumba kimoja, 40 za chumba kimoja cha malazi na nyingine 40 za vyumba viwili vya malazi ambazo zitauzwa kwa bei ya milioni 1.58, 2.5 na 3.52 mtawalia.
Unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali kuu kupitia kwa shirika na kitaifa la nyumba NHC na serikali ya kaunti ya Homabay.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Gavana Wanga alisema serikali ya kaunti imejitolea kujenga nyumba za gharama nafuu kwa lengo la kuhakikisha familia za mapato ya chini zinapata makazi mazuri na ya gharama nafuu.
Wanga alishukuru kwa utambuzi huo kimataifa akiutaja kuwa dhihirisho kwamba wako tayari kama serikali ya kaunti kushirikiana na washirika wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo.
Dennis Papa Odenyi Quansah mwakilishi wa shirika la IFC EDGE Kenya aliyempokeza Wanga cheti hicho alisema mradi wa Homabay ndio wa kwanza kuidhinishwa na anatumai kwamba makundi mengine ya IFC yanayounga mkono miradi ya nyumba za bei nafuu kuhamasisha kuhusu mbinu za ujenzi zinazozingatia utunzi wa mazingira na matumizi ya nishati.
Mkurugenzi mtendaji wa NHC David Mathu alisema idhinisho hilo sio cheti tu bali ni ishara ya juhudi za kutunza mazingira ambazo zitaathiri kwa njia nzuri wakazi wa nyumba hizo na jamii kwa jumla.