Familia ya mwigizaji wa Nollywood nchini Nigeria John Okafor maarufu kama Mr. Ibu imetangaza kwamba amekatwa mguu anapoendelea kupokea matibabu.
Tangazo hilo liliwekwa kwenye akaunti yake ya Instagram na linasema kwamba kufikia sasa mwigizaji huyo amefanyiwa upasuaji mara saba, mojawapo ikiwa kukatwa mguu.
Mwandishi wa taarifa hiyo ambaye anamrejelea Okafor kama “Baba” anashukuru umma kwa mchango wa kugharamia matibabu ya mzee huyo akielezea kwamba ilikuwa muhimu akatwe mguu ili kuongeza uwezekano wake kuendelea kuishi.
Aliendelea kuhimiza watu wenye nia njema waendelee kutuma michango yao kwani wanaihitaji sana kama familia ili kuendelea kugharamia matibabu ya Mr. Ibu.
Awali Ibu mwenyewe alionekana kwenye video akiomba mchango ambapo alionekana kuhofia kwamba huenda akakatwa mguu na sasa hilo limetimia.
Kabla ya hapo alionekana akisherehekea siku ya kuzaliwa hospitalini ambapo alitimiza umri wa miaka 62.