Moto wawaacha watu zaidi ya 200 bila makazi Nyahururu

Martin Mwanje
1 Min Read

Watu zaidi ya 200 wameachawa bila makazi baada ya moto kuzuka katika mtaa wa mabanda wa Maina viungani mwa mji wa Nyahururu.

Wakazi waliozungumza na wanahabari, wakiongozwa na mwenyekiti wa Nyumba Kumi Macharia Kahwai, wamesema moto huo ulianzia kwenye nyumba moja ya mbao katika hali isiyoeleweka.

Kahwai amesema wakazi walijaribu kuokoa mali yao bila mafanikio kwani moto huo uliozuka saa 10 alfajiri ulienea kwa kasi.

Waathiriwa sasa wanaitaka serikali kuu na viongozi wa eneo hilo kuwasaidia kwa kuwapatia chakula, malazi, mavazi na vyombo vya kupikia miongoni mwa bidhaa zingine.

Pia walimnyoshea kidole cha lawama mwanakandarasi anayetengeneza njia zinazoingi kwenye barabara kuu katika mtaa huo wa mabanda kwa kushindwa kutengeneza njia mbadala za matumizi. Kulingana nao, hali hiyo ilisababisha gari la zimamoto kukawia kwani lililazimika kutumia njia ndefu kufika eneo la mkasa huo.

Wakazi hao wanasema hiki ni kisa cha 11 cha kuzuka kwa moto katika eneo hilo mwaka huu.

Aidha wamewataka viongozi wa eneo hilo kutimiza ahadi zao ambazo wamekuwa wakiahidi bila kuzitekeleza.

TAGGED:
Share This Article