Moses Kuria akabidhi rasmi Wizara ya Biashara kwa Rebecca Miano

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri Moses Kuria leo Jumatano amemkabidhi rasmi Waziri Rebecca Miano Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Kuria anasema miezi 11 iliyopita imekuwa ya kufana kwake na kwa wenzake katika Wizara ya Biashara ambapo alijikakamua kuibadilisha ili iwiane na ajenda kuu ya serikali ya Kenya Kwanza.

Anasema anaamini ameweka msingi thabiti na sasa nchi iko mahali pazuri pa kubadilika kiuchumi.

“Uzalishaji tayari umeanza na sasa wawekezaji wako tayari kuanzisha viwanda katika sehemu mbalimbali za nchi ambako tumezindua maeneo ya viwanda,” alisema Kuria.

Anamshukuru Rais William Ruto kwa jukumu jipya ambalo alimteua kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma akisema anakwenda huko kuongoza kama mratibu wa miradi inayohusisha wizara zaidi ya moja na kuondoa vikwazo vya utekelezaji wa haraka wa miradi na utoaji huduma kwa Wakenya.

Rais Ruto alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri Jumatano wiki iliyopita ambapo Kuria alihamishwa kutoka Wizara ya Biashara hadi ile ya Utumishi wa Umma, nafasi yake ikichukuliwa na Waziri Miano.

Penina Malonza anachukua mahali pa Miano katika Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wengine waliohamishwa ni Waziri Alice Wahome kutoka Wizara ya Maji hadi Wizara ya Ardhi na Ujenzi wa Nyumba, wadhifa wake ukichukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi Zacharia Mwangi.

Aisha Jumwa sasa ni Waziri wa Masuala ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi baada ya wizara yake ya awali kugawanywa mara mbili ili kubuni wizara ya Utumishi wa Umma.

Dkt. Alfred Mutua sasa ni Waziri wa Utali,i wadhifa ulioshikiliwa na Penina Malonza. Wizara ya Mambo ya Nje ambayo aliisimamia awali ilihamishiwa kwenye Afisi ya Waziri aliye na Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi.

Share This Article