Moroto ataka maafisa wa usalama washughulikie wizi wa pikipiki

Marion Bosire
2 Min Read

Mbunge wa eneo la Kapenguria lililo katika kaunti ya Pokot Magharibi Samuel Moroto amewataka maafisa wa usalama wa kaunti hiyo kushughulikia tatizo la wizi wa pikipiki.

Moroto aliyekuwa akihutubia hafla moja katika eneo bunge lake alishangaa jinsi wizi huo unaendelea ilhali hakuna yeyote aliyetiwa mbaroni hadi sasa.

Alitoa changamoto kwa maafisa wa usalama wa kaunti hiyo kuharakisha uchunguzi kuhusu wizi wa jumla ya pikipiki 72 kufikia sasa.

Pikipiki hizo ni za vijana wanaozitumia kusafirisha abiria na zote ziliibwa katika kipindi cha mwezi mmoja pekee.

Mmoja wa viongozi wa chama cha waendesha boda boda wa eneo hilo aliyezungumza kwenye hafla hiyo alisema kwamba hata ingawa ana wadhifa wa uongozi hana ufadhili unaohitajika.

Alisema kinapotokea kisa cha wizi wa pikipiki inakuwa vigumu kwake na wenzake kufuatilia kwa kukosa usaidizi muhimu kama vile mafuta.

Wizi wa piki piki ni tatizo kubwa nchini Kenya ambapo shirikisho la usalama wa waendesha Boda Boda nchini lilitangaza mwezi Julai mwaka huu kwamba linapanga kusajili waendesha boda boda wote nchini kama njia ya kutokomeza tatizo hilo.

Mwenyekiti wa kitaifa wa shirikisho hilo Kevin Mubadi alifichua kwamba usajili huo utabuni mfumo mpana wa wasifu wa wahudumu hao wa boda boda, nambari za pikipiki zao na maeneo wanayohudumu.

Anaamini usajili huo utasaidia umma kuripoti kuhusu pikipiki yoyote inayoshukiwa kuibwa kwa maafisa wa usalama.

Share This Article