Moraa atwaa dhahabu ya mita 800 mashindano ya Riadha ya Dunia

Dismas Otuke
2 Min Read

Mary Moraa ndiye bingwa mpya wa dunia katika mbio za mita 800 na Mkenya wa tatu kushinda dhahabu ya dunia kwa wanawake.

Moraa aliishindia Kenya dhahabu ya tatu Jumapili usiku katika siku ya mwisho ya makala ya 19 ya mashindano ya Riadha ya Dunia mjini Budapest nchini Hungary.

Moraa alijakakamua akiziparakasa mbio hizo kwa dakika 1 sekunde 56 nukta 03.

Moraa ambaye pia ni bingwa wa jumuiya ya madola anajiunga na Janeth Jepkosgei bingwa wa mwaka 2007 na Eunice Sum bingwa wa mwaka 2013, kuwa washindi wa Kenya katika mashindano ya dunia.

Keely Hodgkinson wa Uingereza alinyakua nishani ya fedha kwa dakika sekunde 56 nukta 34 naye Athing Mu wa Marekani akashinda shaba.

Jacob Krop alishinda nishani ya shaba ya mita 5,000 kwa muda dakika 13 sekunde 12 nukta 28.

Yakub Ingebrigtsen wa Norway alishinda dhahabu naye Mohamed Katir wa Uhispania akanyakua nishani ya fedha.

Katika mita 3000 kuruka viunzi na maji, Beatrice Chepkoech alizidiwa maarifa katika mita 100 za mwisho na kumaliza wa pili kwa muda wa dakika 8 sekunde 58 nukta 98.

Winfred Mutile Yavi wa Bahrain aliinyakulia Bahrain dhahabu akitumia dakika 8 sekunde 54 nukta 29.

Kenya ilimaliza ya tano na ya kwanza Afrika kwa medali 10 dhahabu 3 fedha 3 na shaba 4.

Marekani iliongoza kwa medali 29, dhahabu 12, fedha 8 na shaba 9 ikifuatwa na Canada kwa dhahabu 4 na fedha 2 huku Uhispania ikichukua nafasi ya tatu kwa dhahabu 4 na fedha1.

Tokyo itaandaa makala ya 20 ya mwaka 2025.

Share This Article