Halmashauri ya Chama cha Raga nchini—KRU, imempiga marufuku mwenyekiti Alexnder Kiplagat Mutai kwa utovu wa nidhamu.
Kwenye kikao kilichoandaliwa jana Machi 6, wanachama wa bodi hiyo kwa kauli moja waliafikiana kumzuia Mutai kujihusisha na shughuli zozote za KRU, akisubiri uamuzi wa mkutano mkuu ulioratibiwa kuandaliwa tarehe 24 mwezi huu.
KRU kwenye taarifa kwa vyombo vya habari leo imeahidi kudumisha hadhi ya usimamizi wake na kuhakisha mzozo uliopo hautaathiri shughuli zake.
Ingawa haijewekwa paruwanja kiini cha adhabu hiyo ya Mutai, yamkini kumekuwa na mvutano na mfarakano kati yake na maafisa wengine watatu waliochaguliwa pamoja na wanachama wengine wa KRU.
Ni mara ya pili ambapo jaribio la kumng’atua afisini Mutai litakuwa likiwasilishwa tangu ashike hatamu za uongozi mwaka 2023, baada ya jaribio la kwanza kufeli mwaka uliopita.
Kumeibuka makundi mawili yanayozozania uongozi wa KRU, hali ambayo inatishia kusambaratisha chama hicho.