Naibu Gavana wa kaunti ya Kisii Dkt. Robert Monda alikanusha mashtaka yote manne yanayomkabili alipofika mbele ya bunge la Seneti jana Jumatano.
Kwenye kesi iliyowasilishwa na bunge la kaunti ya Kisii, Dkt. Monda anashtakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi, kukiuka katiba, kukosa maadili na kutekeleza uhalifu.
Kadhalika bunge hilo linamshtaki kwa kuitisha hongo ya shilingi laki nane kutoka kwa mmoja wa wakazi ili amsaidie kupata ajira kwa mwanawe wa kiume.
Naibu Gavana huyo pia anadaiwa kuwatumia polisi wa ofisi kufanya kazi katika shamba lake katika kaunti ya Kisii.
Utetezi wa Dkt. Monda unaongozwa na wakili Katwa Kigen na kinara wa walio wengi katika bunge la kitaifa Sylvanus Osoro pamoja na mashahidi sita.
Kwa upande mwingine, utetezi wa bunge la kaunti ya Kisii unaongozwa na wakili Ndegwa Njiru.
Kesi hiyo itakamilika Alhamisi ikiwa ni siku ya pili ya kusikizwa kwake kabla ya bunge la Seneti kutoa uamuzi.