Mwigizaji na mwandaaji wa filamu za Nigeria Nollywood Monalisa Chinda ametangaza kifo cha mamake mzazi kupitia kwa akaunti yake ya Instagram.
Mona alichapisha picha ya mshumaa na kuandika, “Lala salama mama, Dame Comfort Franca Chinda. Utasalia kwenye nyoyo zetu milele. Nashukuru kwa muda tuliokuwa pamoja.”
Chinda ambaye pia ni mwanahabari aliendelea kumsifia marehemu mamake akigusia kujitolea kwake kwa familia, mapenzi aliyokuwa nayo kwao na kwa hulka njema aliyoweka ndani yao kupitia malezi mema.
Mwigizaji huyo hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu kilichosababisha kifo cha mamake mzazi na alikokufia.
Taarifa hizo zimegusa waigizaji wenzake ambao wanamtumia jumbe za pole mitandaoni. Uche Obodo hakuamini taarifa hizo na akataka kujua jinsi anazichukulia.
“Naomba nafsi ya mama ilale salama. Nitakupigia simu hivi karibuni.” alimalizia Obodo katika ujumbe wake.
Eucharia Anunobi aliandika, “Ni salama kwako na kwa familia yako”, Freddie Leonard akatoa rambi rambi zake huku mwandaaji wa filamu Uduak Isong akiandika, “Pole sana kwa hili, Lisa. Naomba roho yake ipumzike salama”.
Monalisa Chinda wa umri wa miaka 50 sasa ni mzaliwa wa eneo la Port Harcourt, jimbo la Rivers nchini Nigeria na amekuwa akiigiza kwa miaka 29 sasa.
Sio mengi yanafahamika na umma kuhusu familia yake.