Mombasa Combined kuwania mataji ya Afrika Mashariki

Tom Mathinji
1 Min Read
Timu ya ndondi ya Mombasa Combined.

Timu ya ndondi ya Mombasa Combined itashiriki katika mapigano baina ya vilabu, kuwania mataji ya kanda ya Afrika mashariki.

Akizungumza mjini Mombasa wakati timu hiyo ilipoondoka kuelekea Jijini Tanga nchini Tanzania, Kocha Mkuu Peter Onyango alisema timu hiyo imejiandaa vilivyo kushiriki katika mapigano hayo.

“Tunatarajia matokeo mema katika mashindano hayo Jijini Tanga. Wanandondi wangu wamekuwa wakifanya mazoezi kujiandaa kwa michuano hiyo na nina imani watashinda medali katika mashindano hayo,” alisema Onyango.

Kocha huyo aliongeza kuwa jumla ya mabondia kumi na sita wa humu nchini watashiriki katika mapigano hayo ya siku nne, ambayo pia yamezileta pamoja washiriki kutoka Afrika Kusini na Malawi.

Aliongeza kuwa makala ya mwaka huu yatajumuisha maoigano ya chipukizi kama sehemu ya kuwapa uzoevu mabondia wachanga.

Hii ni mara ya tatu kwa timu ya Mombasa Combined kushiriki katika mapigano hayo baada ya kujinyakulia medali mbili za dhahabu katika makala mbili yaliyopita.

Share This Article