Mnangagwa aapisha mwanawe na mpwa wake

Marion Bosire
2 Min Read
David Kudakwashe akiapishwa kuwa waziri msaidizi wa fedha

Hata baada ya kushtumiwa vikali na upande wa upinzani nchini Zimbabwe, Rais wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa, ameapisha mwanawe na mpwa wake kuhudumu kwenye nyadhifa za mawaziri wasaidizi.

Shughuli ya kuapisha mawaziri na mawaziri wasaidizi iliandaliwa Jumanne katika mji mkuu wa nchi hiyo Harare ambapo mawaziri zaidi ya 20 na mawaziri wasaidizi zaidi ya 10 waliapishwa.

Mwanawe Mnangagwa kwa jina David Kudakwashe wa umri wa miaka 34, aliteuliwa kuhudumu kama waziri msaidizi katika wizara ya fedha huku mpwa wake Tongai Mnangagwa wa miaka 45, akiteuliwa kuhudumu kama waziri msaidizi katika wizara ya utalii.

Akizungumza na wanahabari, David alisema kwamba hakutarajia kuteuliwa kwa wadhifa huo na taarifa hiyo ilikuwa ya kushtukizia. Atahudumu chini ya waziri wa fedha Mthuli Ncube.

Wakosoaji wa serikali ya Mnangagwa wanasema kwamba Ncube amesimamia kile wanachokitaja kuwa kuangamia kwa nchi hiyo kiuchumu na mfumuko wa kiwango cha juu zaidi wa bei za bidhaa.

Chama cha Mnangagwa cha ZANU-PF kimeongoza nchi hiyo ya Zimbabwe kwa zaidi ya miongo minne. Yeye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2017 wakati mtangulizi wake Robert Mugabe alibanduliwa madarakani kupitia mapinduzi.

Mwaka mmoja baadaye akawania urais na kuibuka mshindi.

Alichaguliwa tena kwa muhula wa pili Agosti 23, 2023 kwa asilimia 52.6 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake Nelson Chamisa akipata asilimia 44.

Share This Article