Mkuu wa vikosi vya ulinzi Francis Ogolla amefariki

Tom Mathinji
2 Min Read
Mkuu wa vikosi vya ulinzi KDF, Jenerali Francis Ogolla ameaga dunia.

Mkuu wa vikosi vya ulinzi hapa nchini KDF Jenerali Francis Ogolla, ameaga dunia leo Alhamisi katika ajali ya ndege eneo la Sindar kaunti ya Elgeiyo Marakwet.

Akihutubia taifa Alhamisi usiku katika ikulu ya Nairobi,  Rais William Ruto alisema maafisa wengine tisa wa kijeshi walifariki katika ajali hiyo.

Kulingana na kiongozi wa taifa, maafisa wawili wa kijeshi walinusurika katika ajali hiyo na wanapokea matibabu hospitalini.

Waliofariki na Jenerali Ogolla ni pamoja na:

1. Brigadier Swale Saidi,
2. Colonel Duncan Keittany,
3. Lieutenant Colonel David Sawe,
4. Major George Benson Magondu,
5. Captain Sora Mohamed,
6. Captain Hillary Litali,
7. Senior Sergeant John Kinyua Mureithi,
8. Sergeant Cliphonce Omondi, na
9. Sergeant Rose Nyawira.

Jenerali Ogolla ambaye alikuwa katika helikopta aina ya Huey, alikuwa ameondoka Jijini Nairobi Leo Alhamisi asubuhi, kuwatembelea wanajeshi ambao wanahudumu eneo la North Rift chini ya operesheni ya Maliza Uhalifu, pamoja na kukagua shughuli za ukarabati wa shule katika eneo hilo.

“Natuma risala za rambirambi kwa familia wanaoomboleza. Mungu apatie familia hizo amani wakati huu wa majonzi. Vile vile nawatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa katika ajali hiyo,” alisema Rais Ruto.

Kufuatia kifo cha Ogolla, Rais ametangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa, huku bendera ya taifa, ya jeshi na ile ya Afrika Mashariki zipeperushwe nusu mlingoti kuanzia kesho Ijumaa Aprili, 19, 2023.

Share This Article