Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN Antonio Guterres amewasili nchini Urusi leo Jumatano kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa BRICS.
Hiyo ni ziara yake ya kwanza nchini humo katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili ambacho kimeibua shutuma kutoka kwa Ukraine.
Mkutano huo ndilo kongamano kubwa zaidi la kidiplmasia nchini Urusi tangu nchi hiyo ilipoanzisha operesheni yake kamili ya kijeshi nchini Ukraine mwaka 2022.
Rais Vladimir Putin anataka kuutumia mkutano huo kudhihirisha kuwa majaribio ya kumtenga kwenye jukwaa la kimataifa yameshindikana.
Viongozi wapatao 20 wa dunia, wakiwemo viongozi wa China, India, Uturuki na Iran, wapo katika mji wa katikati mwa Urusi wa Kazan. Wakiwa mjini humo, wataangazia mada kama vile kuendeleza mfumo wa kimataifa wa malipo unaoongozwa na BRICS na mgogoro Mashariki ya Kati.
Urusi inauchukulia mkutano huo kuwa mbadala wa mashirika ya kimataifa yanayoongozwa na nchi za Magharibi kama vile G7 — msimamo ambao unaungwa mkono na Rais wa China Xi Jinping.
Katika mazungumzo ya pande mbili jana Jumanne, ikiwa ni pamoja na mazungumzo kati yake na Xi na Waziri Mku wa India Narendra Modi, Putin alipongeza uhusiano wa karibu na “ushirikiano wa kimkakati” wa Urusi na washirika wake.
Guterres atafanya mazungumzo na Putin kesho Alhamisi ambapo wawili hao watajadili mgogoro wa Ukraine, kwa mujibu wa Ikulu ya Urusi.
Ukraine imelaani ziara ya Guterres nchini Urusi.