Mkuu wa IOM kutembelea Kenya mwezi Oktoba

Martin Mwanje
1 Min Read
Mkurugenzi Mkuu wa IOM Amy Pope

Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM amepangiwa kufanya ziara ya siku mbili nchini Kenya. 

Amy Pope atafanya ziara ya siku mbili nchini humo kuanzia Oktoba 12-14, 2023.

Hiyo itakuwa ziara yake ya kwanza nchini Kenya tangu alipochaguliwa kuhudumu kwa muhula wa miaka mitano katika wadhifa huo.

Pope aliandikisha historia alipochaguliwa Mei 15, 2023 kama mwanamke wa kwanza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa IOM katika kipindi cha miaka 72.

Akiwa nchini humo, Pope ambaye ni raia wa Marekani, atafanya mazungumzo na Rais William Ruto na maafisa wengine wakuu serikalini.

“Mazungumzo kati yao yataangazia uongezaji wa ushirikiano wa IOM katika kuhamasisha uhamiaji salama, wa mara kwa mara na wenye heshima, na kuangazia changamoto za uhamiaji nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na uhamiaji unaotokana na mabadiliako ya tabia nchi,” inasema IOM katika taarifa.

Wahamiaji wapatao milioni 1.1 wanaishi nchini Kenya sawia na wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi elfu 490.

Wote hao hufika nchini Kenya kutafuta ustawi bora wa kiuchumi, elimu na afya bora.

IOM imekuwa ikifanya kazi na serikali ya Kenya kuangazia masuala ya wahamiaji kwa takriban miongo 40.

 

 

 

Share This Article