Mkutano wa viongozi wa Bunge la Taifa waanza Naivasha

Marion Bosire
2 Min Read
Moses Wetang'ula - Spika wa Bunge la Taifa

Mkutano wa viongozi wa Bunge la Taifa umeanza leo Jumatatu mjini Naivasha. 

Spika wa bunge hilo Moses Wetang’ula ameuhutubia mkutano huo wa kila mwaka ambao utaandaliwa kati ya leo Jumatatu, Oktoba 28 hadi 30, 2024.

Mada ya mkutano wa mwaka huu ni “kuboresha ushirikiano katika uongozi ili kuharakisha utekelezaji wa jukumu la bunge”. Unalenga kuendelea kujenga kutoka kwa mkutano wa mwaka jana uliolenga kuboresha ajenda ya utunzi wa sheria.

Kulingana na Wetang’ula, mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa viongozi wa bunge kuweka mikakati ya mambo yanayofaa kupatiwa kipaumbele, wanapojiandaa kwa awamu ya nne inayoanza Novemba 5, 2014.

Wadau wa sekta muhimu kama ile ya nishati pia watakuwepo ikitizamiwa kwamba umma umekuwa ukilalamikia gharama ya juu ya umeme na ufaafu wake.

Waziri wa Nishati na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya umeme ya Kenya Power watahudhuria mkutano huo ili kujaribu kutatua matatizo ya Wakenya.

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah, anasema bunge limepiga hatua kubwa tangu lilipobuniwa baada ya uchaguzi wa mwezi Septemba, 2022.

Alielezea kuhusu mipango kadhaa ya uhamasisho ambayo imeandaliwa ili kuwezesha wabunge kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Mkutano huo ambao pia unarejelewa kama utathmini wa katikati ya muhula wa Bunge la Kitaifa, unatoa fursa kwa viongozi wa bunge hilo kutathmini utendakazi na kushughulikia changamoto ibuka.

Washiriki wa mkutano huo wataangazia mikakati ambayo inaweza kutekelezeka ya kuimarisha kazi ya bunge na kazi za kamati mbali mbali za bunge.

Mkutano huo wa siku tatu unaahidi kuwa muhimu kwa bunge huku ukiliandaa kwa utawala bora na hatua zifaazo kwa miezi kadhaa ijayo.

Share This Article