Serikali imesitisha kandarasi ya mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya viwanja vya ndege nchini, Alex Gitari.
Hii ni kufuatia kukatizwa kwa nguvu za umeme katika sehemu nyingi nchini ambapo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta uliathirika pia, huku wasafiri wakikwama gizani kwa muda wa takriban saa mbili.
Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen pia alitangaza kwamba Henry Ogoye ameteuliwa kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa halmashauri hiyo.
Ogoye alikuwa mkuu wa idara ya mipango katika halmashauri hiyo.
Waziri pia alimhamisha meneja wa JKIA Abel Gogo hadi kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mombasa.
Mahala pa Gogo patachukuliwa na meneja wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kisumu, Selina Gor ambaye sasa atasimamia shughuli za kila siku kwenye uwanja wa JKIA.
Peter Wafula aliyekuwa kwenye uwanja wa ndege wa Mombasa amehamishiwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kisumu katika wadhifa huo huo.
Murkomen alifanya mabadiliko hayo baada ya kuzuru uwanja wa ndege wa JKIA Jumamosi asubuhi, kufuatia kukatizwa kwa nguvu za umeme kote nchini jana usiku.
Waziri alisema kuwa utaratibu wa kuweka jenereta ya umeme kwenye uwanja wa ndege wa JKIA utaanza siku ya Jumatatu huku akitoa hakikisho kwamba tukio kama hilo halitajiri tena.