Baraza la Mitihani nchini, KNEC limetangaza kuanza kwa mitihani ya KPSEA na KJSEA leo Jumatatu kote nchini.
Jumla ya watahiniwa 1,298,089 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya 6, KPSEA.
Kwa upande mwingine, watahiniwa 1,130,669 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya 9, KJSEA.
Watahiniwa wa KPSEA kwa leo wanakabiliana na mtihani wa Hisabati na lugha ya Kiingereza huku wale wa KJSEA wakifanya mtihani wa lugha ya Kiingereza ikiwa ni pamoja na uandishi wa insha.
Awali, KNEC iliagiza kontena za mitihani ya KPSEA na KJSEA kufunguliwa saa 12 asubuhi katika vituo vya mitihani.
Wasimamizi wa mitihani hiyo nao wametakiwa kuhakikisha kontena za mitihani sahihi zinafunguliwa ili kukabiliana na mianya yoyote ya wizi wa mitihani.
Simu za mkononi pia zimetakiwa kusamilishwa kwa wasimamizi wa mitihani na kufungiwa mahali pamoja.
Mitihani ya KPSEA na KJSEA inaanza huku mtihani wa kidato cha nne ukiingia wiki ya pili leo Jumatatu.
Kinyume cha KPSEA na KJSEA, KNEC imeangiza kontena za mtihani wa KCSE kufunguliwa saa 1 asubuhi.
Watahiniwa zaidi ya 996,000 wanafanya mtihani wa KCSE mwaka huu.
