Misukosuko inayoghubika michezo ya Olimpiki jijini Paris

Dismas Otuke
2 Min Read

Michezo ya Olimpiki itakayofunguliwa rasmi Ijumaa, imekumbwa na misukosuko mingi kuanzia kwa matayarisho ya miundo mbinu hadi kuelekea uwanjani.

Wafanyikazi wa kuzoa taka jijini Paris walitishia kugoma  wiki mbili zilizopita wakitaka nyongeza ya mshahara.

Baadaye wafanyikazi hao walifutilia mbali mgomo huo baada ya kulpokea malipo yao.

Wapigaji densi walioalikwa kutumbuiza katika sherehe za ufunguzi kesho,walitishia kugoma hadi wakapewa nyongeza ya baina ya shilingi 21,000 na 23,000 .

Hata hivyo wapiga densi hao walitangaza kufutilia mbali mgomo Jumatano wiki hii, baada ya kamati andalizi kukubali kuwapa nyongeza.

Pia kumeripotiwa na visa vya udunguaji wa droni kadhaa za kijasusi nyingi zikiwa za Urusi, zinazoaminika kutumika kuvuruga mashindano hayo.

Maafisa wa usalama hawajatoa taarifa zaidi kuhusu jinsi majasusi hao wa Urusi wanapanga kuvuruga michezo hiyo, ingawa wameweka bayana kuwa haihusikani na shambulizi la kigaidi.

Maafisa wa usalama pia wameendesha msako kukabiliana na uvamizi na ulaghai wa kupitia mitandaoni, huku wakiwaonya watumizi wa tarakilishi kutahadhari dhidi ya udukuzi na uhalifu wa mitandaoni.

Kambi ya wachezaji wa Israel jijini Paris pia imewekwa chini ya ulinzi mkali kuzuia mashambulizi yoyote yanayohusiana na ulipizaji kisasi dhidi ya mashambulizi ya Israel katika eneo la Gaza nchini Palestina.

Hali tete ya kiasa pia iliathari michezo hiyo hali iliyomlazimu Rais Emmanuel Macron kuahirisha kutangaza baraza jipya la Mawaziri hadi baada ya michezo ya Olimpiki kukamilika.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Gabriel Attal pia alijiuzulu siku kumi, kabla ya sherehe za ufunguzi wa mashindano hayo.

Mashabiki pia waliingia uwanjani jana baada ya mechi ya soka kati ya Morocco na Argentina kinyume cha sheria.

Mashabiki hao wa Argentina waliteta kuhusu uamuzi wa refa  wa kukataa bao la kusawazisha la dakika za mwisho la  timu yao kwa kusema lilikuwa la kuotea.

Morocco walisajili ushindi wa mabao 2-1.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *