Misori akosoa jopokazi la marekebisho ya mtaala wa CBC

Dismas Otuke
2 Min Read

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa shule za Upili na Vyuo Nchini (KUPPET)  Maurice Akelo Misori amelishutumu jopokazi lililobuniwa na Rais William Ruto  kutathmini mtaala mpya wa umilisi (CBC) kwa kutepetea na kutoa ripoti hafifu.

Kwenye mahojiano ya kipekee na shirika la KBC, Misori  amesema ripoti iliyokabidhiwa  Rais maajuzi kwenye Ikulu ya Nairobi, ilikosa kuangazia kwa kina mapungufu na mbinu mwafaka za kuboresha mtaala huo huku jopokazi hilo likizingatia zaidi idadi ya masomo kwa wanafunzi pekee.

Misori amelalama kuwa jopokazi hilo lililoongozwa na Profesa Raphael Munavu, liliharakisha mchakato huo na kukosa kujumuisha mapendekezo mengi yaliyotolewa  na umma wakati wa kupokea maoni.

“Nimesikitishwa na jopokazi hili kwani kikubwa walichofanya ni kuharakisha na kutoa ripoti ya haraka kumfurahisha Rais lakini wakasahau mapendekezo mengi yaliyotolewa na wanachi. Ukiangalia CBC imekuwa na mianya mingi tangu ianze kutekelezwa lakini jopokazi halikuangazia uhalisia huo kama kukosekana kwa maabara katika shule za msingi wanakosomea wanafunzi wa Sekondari ya Chini na idadi ya wanafunzi dhidi ya mwalimu mmoja,” alidai Misori.

“Kupunguzwa kwa idadi ya masomo kwa wanafunzi wa CBC hilo walifanya vyema maana mwanzo, mbona wanafunzi wapewe masomo mengi?”

Katibu Mkuu huyo wa KUPPET amelitaka jopokazi hilo kufanya tathmini zaidi na kushirikisha umma kuhakikisha mtaala wa CBC unafaulu.

Jopokazi hilo lilipendekeza kupunguzwa kwa idadi ya  masomo kwa wanafunzi wa sekondari ya chini na juu miongoni mwa mapendekezo mengine kwenye ripoti yake kwa Rais.

Misori pia ameitaka Tume ya Kuwaajiri Walimu Nchini, TSC kuharakisha mazungumzo ya nyongeza mpya ya mishahara ya walimu ili kuwakimu dhidi ya matozo mapya yaliyopitishwa na serikali siku chache zilizopita.

“Mshahara wa walimu umeathirika vibaya na tunataka TSC iharakishe  mazungumzo ya nyongeza ya mishahara kwa walimu ili kuwakimu dhidi ya matozo mapya yaliyoidhinishwa na serikali,” aliongeza Misori.

 

 

Website |  + posts
Share This Article