Miradi ya maji yazinduliwa kuwafaidi wakazi wa Salgaa

KBC Digital
2 Min Read
Waziri wa maji na Mabadiliko ya Tabia Nchi kaunti ya Nakuru Dkt. Nelson Tanui.

Serikali ya kaunti ya Nakuru kwa ushirikiano na shirika la World Vision, zimeshirikiana kutatua tatizo la ukosefu wa maji katika eneo la Salgaa kaunti hiyo.

Kulingana na waziri wa Maji na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa kaunti ya Nakuru Dkt. Nelson Tanui, wakazi wa Salgaa, huteka maji katika mto Rongai, ambayo ni machafu, huku mto huo ukikauka nyakati za kiangazi.

Waziri huyo alisikitikia hali ambapo wanafunzi wa shule hutembea umbali wa hadi kilomita sita kila siku kutafuta maji. Hatua hii kwa mujibu wa Tanui, husababisha baadhi ya wanafunzi kukosa kuhudhuria masomo shuleni.

“Wakazi wa eneo hili wamekabiliwa na hatari ya maambukizi ya magonjwa yanayosababishwa na maji kama vile kipindupindu, homa ya matumbo na kuhara,’ alisema Dkt. Tanui.

Tanui alisema serikali ya kaunti ya Nakuru na shirika la World Vision zimetoa shilingi milioni 60 kila moja kwa ujenzi wa mabwawa ya maji, yanayotarajiwa kufaidi takriban familia 300.

Mkurugenzi Mkuu wa World Vison Hapa nchini Gilbert Kamanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa kitaifa wa shirika la World Vision Kenya Gilbert Kamanga , alitoa wito kwa jamii ya wafanyabiashara kuunga mkono juhudi za shirika hilo, kuhakikisha wakazi wa Salgaa wanapata maji safi.

Shule kadhaa katika eneo la Salgaa zimenufaika na mradi huo wa maji huku wanafunzi 695 kutoka shule za msingi za Mimwaita  na Gicheha sasa wakihudhuria masomo yao kikamilifu kutokana na upatikanaji wa maki.

Wanafunzi wengine 390 katika shule za Kyanet na  Umoja, pia wamenufaika pakubwa na miradi hiyo ya maji kutoka World Vision.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *