Mikutano ya kila mwaka ya AfDB yaanza Nairobi

Marion Bosire
1 Min Read

Mikutano ya kila mwaka ya benki ya maendeleo barani Afrika AfDB mwaka huu wa 2024 imeanza leo katika jumba la KICC jijini Nairobi. Mikutano hiyo inaanza leo Mei 27 na itafikia kikomo Mei 31, 2024.

Mada ya mwaka huu ya mikutano hiyo ni “Mabadiliko ya Afrika, kundi la benki ya maendeleo barani Afrika na mabadiliko ya mfumo wa kifedha ulimwenguni”.

Wawakilishi wa serikali ya Kenya na wa benki hiyo ambayo makao yake makuu yako Abidjan walifanya mikutano kadhaa ya kuandaa mikutano hiyo ambayo ni fursa ya kubadilishana mawazo na ufahamu kati ya waamuzi wakuu barani Afrika.

Katibu wa mipango ya kiuchumi nchini James Muhati aliongoza ujumbe wa Kenya kwenye mkutano ulioandaliwa katika jumba la KICC Mei 2, 2024 ambapo alisema kwamba maandalizi yalikuwa yanaendelea ipasavyo.

Viongozi wa nchi wapatao 28 wanatarajiwa kuhudhuria mikutano hiyo ambayo pia inatarajiwa kuhudhuriwa na magavana na mawaziri wa fedha wa nchi za bara hili la Afrika.

Kulingana na benki ya AfDB, mikutano ya mwaka huu inatarajiwa kuimarisha kasi ya mabadiliko muundomsingi barani humu kama njia ya kuharakisha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Share This Article