Miili mitatu imeopolewa kutoka eneo lililofurika la Kona Punda katika barabara ya Garissa –Madogo, eneo ambapo mashua iliyokuwa imewabeba zaidi ya watu 40 kupinduka Jumapili jioni.
Ajali hiyo ilitokea saa kumi na mbili na nusu Jumapili jioni, na hivyo kutatiza maafisa wa shirika la msalaba mwekundu kutoka kaunti za Garissa na Tana River, kutekeleza shughuli za uokoaji kutokana na giza. Hata hivyo shirika hilo liliweza kuwaokoa watu 22.
Kutokana na kufungwa kwa barabara ya Madogo-Garissa, wakazi wa eneo hilo waliazimia kutumia mashua zilizokuwa zikitoza shilingi 1,500 umbali ambao awali ulitozwa shilingi 30 na magari ya uchukuzi..
Mashua hiyo inasemekana ilikuwa imewabeba zaidi ya abiria 40 wakati wa ajali hiyo.
Maafisa wa polisi tayari wamefunga eneo hilo, kuwazuia wakazi kufika katika eneo la mafuriko.