Miili sita yaopolewa kwenye jengo lililoporomoka Eastleigh

Huduma ya Taifa ya Polisi ilisema miili hiyo iliyopatikana sasa inafikisha idadi jumla ya maafa kutoka kwa jengo hilo kuwa nane.

Tom Mathinji
1 Min Read
Miili sita zaidi yapatikana kutoka kwa jengo lililoporomoka Eastleigh.

Kundi la maafisa kutoka asasi mbalimbali linalotekeleza operesheni ya uokoaji kwenye jengo lililoporomoka Eastleigh, limepata miili sita leo Alhamisi kutoka kwa vifusi vya jengo hilo.

Kupitia kwenye ukurasa wa X, Huduma ya Taifa ya Polisi ilisema miili hiyo iliyopatikana sasa inafikisha idadi jumla ya maafa kutoka kwa jengo hilo kuwa nane.

“Watu sita zaidi, wanawake wanne na wanaume wawili, wamepatikana wamefariki leo Novemba 5, 2026 na kufikisha idadi ya waliofariki kuwa nane,” ilisema huduma hiyo.

Huduma hiyo ya Polisi iliwasihi wananchi wanaowatafuta wapendwa wao waliotoweka, kutembelea kituo cha Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo la mkasa au kupiga simu kupitia nambari 1199.

Maafisa kutoka vitengo mbalimbali vya serikali vinaendelea na shughuli za uokoaji kwenye jengo hilo lililoporomoka Oktoba 23, 2026.

Share This Article