Miili minne ya watu wanaoshukiwa kuwa waathiriwa wa mafuriko, imeopolewa kutoka Mto Mathare.
Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku ya Jumanne Jijini Nairobi. Kamanda wa Polisi wa katika kaunti ndogo ya Starehe, Fred Abuga, alisema wanne hao wanajumuisha wanaume wawili na wanawake wawili.
Alisema kuwa watu wengine sita hawajulikani waliko huku shughuli ya kuwatafuta na kuwaokoa manusura ikiendela mtaani Mathare.
Shughuli ya pamoja ya uokoaji inafanywa na serikali ya kaunti ya Nairobi na shirika la msalaba mwekundu.
Watu 18 wakiwemo watu wazima 11 na watoto saba waliokuwa wameathiriwa na mafuriko katika eneo la Mradi huko Mathare 4A waliokolewa Jumatano.
Kwenye taarifa, shirika la msalaba mwekundu limesema kuwa shughuli ya uokoaji ilifanywa na kundi lake maalum ambalo lilianzisha mikakati hiyo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika maeneo mengi jijini Nairobi.
Shirika hilo lilisema kuwa linatekeleza shughuli kama hizo katika maeneo mengine nchini.