Miili minne imeopolewa kutoka kwenye jengo lililoporomoka katika mtaa wa Shauri Moyo, kaunti ndogo ya Kamukunji jana Jumatatu.
Afisa anayesimamia shughuli za uokoaji Dkt. Duncan Ochieng’ alisema miili hiyo ilikuwa ya wanaume.
Ochieng’ alisema watu wengine wanne waliokolewa wakiwa hai kutoka kwenye vifusi vya jengo hilo.
Shughuli kuwatafuta watu wengine wawili zinaendelea.
Kulingana na walioshuhudia mkasa huo, jengo hilo lilibomoka saa nane alasiri siku ya Jumatatu.
Jengo hilo ni miongoni mwa yale yaliyojengwa karibu na mto Nairobi ambayo yamepangwa kubomolewa chini ya mpango unaoendelea wa usafishaji mto huo.
Vikosi vya Ulinzi nchini, KDF, Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS, maafisa wa utawala wa serikali kuu na Shirika la Msalaba Mwekundu ni miongoni mwa waliotumwa eneo la tukio kusaidia katika shughuli za utafutaji na uokozi.
Watu wametakiwa kutokaribia eneo hilo ili kuruhusu shughuli za utafutaji na uokozi kuendelea bila vizuizi.