Miili 33 imepatikana kwenye kaburi la pamoja kaunti ya Kericho, 25 ikiwa ya watoto na 8 ya watu wazima.
Shughuli ya ufukuaji wa miili hiyo iliongozwa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Awali, ililenga miili 14 ambayo iliaminika kuzikwa kisiri katika eneo hilo.
Maafisa wa uchunguzi baadaye walibainisha kuwa miili hiyo ilisafirishwa kutoka Hopitali ya Rufaa ya Nyamira, baada ya kukosa kuchukuliwa kwa muda mrefu kutoka chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.
Watu wawili wamekamatwa kuhusiana na sakata hiyo. Wao ni afisa wa Afya ya Umma wa kaunti ya Nyamira na mlinzi wa makaburi ya umma ambako miili hiyo ilizikwa, na wanawasaidia maafisa wa polisi kwa uchunguzi.
Uchunguzi wa maiti unatarajiwa kufanyiwa miili hiyo leo Jumatano kubaini chanzo cha kifo na kufanikisha kuitambua.
Hali ya usalama imeimarishwa katika eneo hilo, ambalo limezingirwa tangu shughuli hiyo ilipoanza.