Migosi asema serikali imejitolea kuhakikisha elimu bora

Marion Bosire
2 Min Read
Julius Ogamba, Waziri wa Elimu

Waziri wa elimu Julius Migosi Ogamba amesema kwamba serikali imejitolea kuhakikisha inatoa elimu inayopatikana, bora na inayofaa kwa wakenya katika viwango vyote.

Migosi alizungumza hayo katika afisi za taasisi ya kukuza mitaala nchini KICD wakati wa kuzindua usambazaji wa vitabu vya kiada vya gredi ya 9 kwenye Junior Secondary, pamoja na vya gredi ya kwanza hadi sita katika shule za msingi.

Alisisitiza kujitolea kwa serikali kuwapa wanafunzi vitabu vya kianda na kwamba katika siku za usoni itahakikisha kila mwanafunzi anapata nakala yake binafsi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa KICD Charles Ong’ondo alisema Kenya ndiyo nchi ya tatu barani Afrika ambayo imetoa vitabu vya kiada bila malipo kwa wanafunzi.

Nchi zilizotangulia kufanya hivyo ni Misri ikifuatiwa na Afrika Kusini.

Mwenyekiti wa KICD Simon Gicharu kwa upande wake aliwataka wadau wa elimu kutochoka kusaidia wanafunzi ili hatimaye waafikie uwezo wao kamili na wajenge jamii yenye maadili.

Waziri Migosi pia aliongoza uzinduzi wa mpango wa kimkakati wa KICD wa mwaka 2023 hadi 2027 huku akipongeza baraza kuu la taasisi hiyo ya mitaala kwa kuutayarisha.

Kulingana naye, mpango huo unaangazia masuala muhimu yanayohusu mamlaka ya taasisi ya KICD na kuorodhesha mikakati ya kuhakikisha inatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Katibu wa elimu ya msingi Belio Kipsang alihudhuria hafla hiyo.

Share This Article