Kaunti ya Kakamega itakuwa mwenyeji wa michezo ya kicosca mwezi huu huku gavana wa Kaunti hiyo, Fernandes Barasa, akiteuliwa kinara wa michezo ya Serikali za Magatuzi nchini inayojulikana kama KICOSCA.
Akikabidhiwa wadhifa huo rasmi na usimamizi wa michezo hiyo mjini Kakamega kutoka kwa mwenzake, Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza, Gavana Barasa amewahakikishia Wakenya kuwa michezo hiyo, iliyoratibiwa kuanza tarehe 20 mwezi huu, itakuwa na usalama wa kutosha.
Naye mwenzake wa Pokot Magharibi, Simon Kachapin, ameonyesha imani yake kwa Barasa, akisema kuwa michezo hiyo itachangia pakubwa katika kukuza talanta za vijana na kuunganisha serikali zote za kaunti.
Michezo hiyo ni ya kumi na moja tangu kuanzishwa kwa mashindano ya KICOSCA chini ya katiba mpya, ikichukua nafasi ya zile za Serikali za Manispaa.