Michael Jordan ambaye awali alikuwa mchezaji wa mpira wa kikapu anasemekana kuendeleza mpango wa kuuza hisa nyingi za timu ya mpira wa kikapu ambayo amekuwa akimiliki ya Charlotte Hornets.
Jordan anauza hisa zake kwa kundi moja la uwekezaji linaloongozwa na Gabe Plotkin na Rick Schnall, haya ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa timu hiyo.
Plotkin amekuwa mmoja wa wenye hisa wa timu hiyo tangu mwaka 2019 kwa kiwango kidogo cha hisa naye Schnall amekuwa na kiwango kidogo cha hisa kwenye timu ya Atlanta Hawks tangu mwaka 2015 hisa ambazo anatafuta kuuza.
Muda wa bodi ya magavana ya ligi ya NBA kukamilisha mauzo hayo ya hisa haujulikani. Jordan anapanga kusalia na kiasi kidogo cha hisa za timu ya Charlotte Hornets aliyoinunua mwaka 2010 kwa Dola milioni 275.
Adam Silver ambaye ni kamishna wa ligi ya NBA alielezea kwamba Michael Jordan, ana haki ya kuuza hisa zake wakati wowote. Kulingana naye thamani ya timu imekua sana tangu Jordan aliponunua Hornets.