Mialiko ya arusi ya Bahati yaanza kununuliwa

Kenyan Prince na Victor Kanyari wanaripotiwa kununua mialiko shilingi milioni 1 kila mmoja.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Kenya Bahati na mkewe, Diana Marua, wameanza kuuza mialiko huku maandalizi ya harusi yao inayotarajiwa ya kifahari yakiendelea.

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Novemba 6, 2026, huku kukiwa na mjadala wa umma kuhusu gharama ya Shilingi milioni 1 kwa kila mwaliko.

Wawili hao walitangaza hafla hiyo Oktoba 7 walipoadhimisha miaka 10 ya kuwa pamoja, wakifichua kuwa sherehe hiyo itahudhuriwa na wageni 100 pekee, huku kila mtu akitakiwa kulipa milioni 1 ili kupata mwaliko.

Tangazo hilo lilizua maoni tofauti mitandaoni, huku baadhi ya Wakenya wakihoji gharama kubwa ya kuhudhuria hafla hiyo, wengine wakiona mpango huo kama sherehe ya kipekee kwa watu wenye uwezo mkubwa kifedha.

Licha ya ukosoaji huo, Bahati ametetea gharama hiyo, akieleza kuwa inalenga watu wenye uwezo wa kifedha, maarufu kama “ballers,” akiwapa changamoto wanaotarajia kuwa bei ya mwaliko itapunguzwa.

Oktoba 13, Bahati alitangaza kuwa mfanyabiashara wa ubadilishanaji wa fedha za kigeni, Kenyan Prince, alinunua mwaliko, akimtaja kuwa mfanyabiashara wa kwanza katika sekta hiyo kupata nafasi katika hafla hiyo.

Mhubiri Victor Kanyari, ambaye awali alikuwa amekosoa bei ya mwaliko huo, pia anaripotiwa kununua mwaliko baada ya kukutana na Bahati Oktoba 13.

Maendeleo hayo yameongeza sura mpya katika mjadala kuhusu mipango ya wanandoa hao, iliyovutia umakini mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Ingawa kila mwaliko unauzwa kwa Shilingi milioni 1 na idadi ya wageni imewekewa kikomo cha 100, wanandoa hao hawajathibitisha hadharani kuwa mialiko yote iliyopo imeuzwa.

Share This Article