Mgomo wa walimu kuanza Jumatatu

Marion Bosire
1 Min Read
Collins Oyuu, katibu mkuu wa KNUT

Mgomo wa walimu ambao umepangiwa kuanza Jumatatu, Agosti 26, 2024 utaendelea kama ilivyopangwa.

Hii ni baada ya viongozi wa vyama vya walimu kukosa kuafikiana na Tume ya Kuajiri Walimu nchini, TSC.

TSC ilikuwa imealika viongozi wa vyama vya KUPPET na KNUT kwa mkutano katika taasisi ya mafunzo ya serikali huko Lower Kabete kujaribu kuepusha mgomo huo lakini hilo halikufanyika.

Kulingana na viongozi wa walimu, TSC ilikubali kutekeleza awamu ya pili ya makubaliano ya pamoja ya mwaka 2021 hadi 2025 lakini ikakosa kujitolea kushughulikia malalamishi yao mengine.

Walimu walitangaza mgomo huo kufuatia hatua ya serikali ya kukosa kutekeleza makubaliano hayo ya nyongeza ya mishahara lakini pia wanataka walimu wa Junior Secondary waajiriwe kwa masharti ya kudumu.

Wanataka pia kwamba serikali iajiri walimu elfu 20 zaidi kwa masharti ya kudumu.

Wametoa ushauri wa wazazi kutorejesha wanao shuleni ifikapo Jumatatu, wakati ambao wanafungua kwa muhula wa tatu na wa mwisho mwaka huu.

Awali, Waziri wa Leba Dkt. Alfred Mutua alifanya mkutano na viongozi wa vyama mbalimbali vya walimu kujaribu kufutilia mbali mgomo uliopangwa lakini hakutoa taarifa kuhusu waliyoafikia.

Share This Article