Mgao wa fedha za kaunti: Mbadi amlimbikizia lawama Mdibiti wa Bajeti

Martin Mwanje
2 Min Read
Dkt. Margaret Nyakang'o - Mdhibiti wa Bajeti

Mdhibiti wa Bajeti Dkt. Margaret Nyakang’o ndiye anayepaswa kulaumiwa kutokana na ucheleweshaji wa mara kwa mara wa fedha za kaunti zilizotolewa na serikali kuu. 

Magavana wamekuwa wakiilaumu Wizara ya Fedha wakidai imekuwa na tabia ya kuchelewa utoaji wa fedha hizo na hivyo kuathiri mno utoaji huduma kwa raia.

Katika baadhi ya kaunti, serikali hata zimeshindwa au kuchelewa kuwalipa wafanyakazi kwa miezi kadhaa na kusababisha migomo hasa ya wahudumu wa afya.

“Natamani Mdhibiti wa Bajeti angekuwa hapa. Nina shida na ofisi yake. Mimi sipendi kuficha mambo. Nayasema yalivyo,” alisema Mbadi wakati wa mkutano wa ushauriano na Magavana mjini Naivasha jana Alhamisi.

“Punde tukitoa fedha kwa kaunti, wacha fedha hizo zifikie kaunti, hatupaswi kuwa na vikwazo. Hakuna sababu Magavana kwamba maafisa wenu daima huwa Nairobi ili kutafuta idhini ya Ofisi ya Mdhibiti wa Bajeti. Hiyo ni njia moja ya kujitafutia fedha na lazima tabia hiyo ikome.”

Ingawa Magavana wanataka kaunti kupatiwa shilingi bilioni 400, Mbadi ameshikilia kuwa serikali kuu inaweza tu kuzipatia shilingi bilioni 380 kutokana na changamoto za kiuchumi zinazoshuhudiwa nchini kwa sasa.

Ili kusaidia kupunguza matumizi ya serikali za kaunti, Waziri aewataka Magavana kufutilia mbali ofisi nyingi walizobuni na kupunguza idadi ya wafanyakazi wao hasa washauri wengi waliowaajiri na ambao amesema hawana manufaa yoyote kwa ustawi wa kaunti.

Website |  + posts
Share This Article