Mtangazaji wa shirika la KBC Simeone Mfumu Kibangu, ndiye mshindi wa tuzo ya mpiga muziki wa rhumba bora redioni na kwenye runinga katika eneo la Afrika Mashariki, kwenye tuzo za E360.
Kibangu ametambuliwa kwa kazi yake ya miaka mingi katika shirika la KBC ambapo amekuwa akiendesha kipindi cha Bridge Over DRC, kinachohusika na burudani ya muziki wa Congo.
Kipindi hicho ambacho pia kinahusisha maelezo kuhusu maana ya nyimbo hizo za kutoka Congo, kilianzia kwenye redio ya KBC inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya kiingereza kabla ya kupelekwa kwenye runinga ya KBC pia.
Hafla ya kugawa tuzo za E360 iliandaliwa Ijumaa Machi 7, 2025 katika ukumbi wa Nairobi Cinema na hii ilikuwa awamu ya 6 ya tuzo hizo.