Mfumo wa ukusanyaji takwimu wa KIAMIS wafanikisha kilimo nchini

Tom Mathinji
2 Min Read

Baada ya kuzinduliwa kwa mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa takwimu almaarufu KIAMIS, waziri wa kilimo na ustawishaji mifugo Dkt. Andrew Karanja, alisema mfumo huo umeimarisha utoaji maamuzi, uwazi na uvumbuzi katika sekta ya kilimo hapa nchini.

Kulingana na waziri huyo, mkakati huo wa ukusanyaji takwimu, umesaidia pakubwa katika juhudi kabambe za kufanyia marekebisho mikakati ya kuhakikisha ukuaji wa sekta ya kilimo.

Kwa upande wake, katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, alielezea malengo makuu ya mkakati huo, yanayojumuisha usimamizi bora wa takwimu,  kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi, za kutegemewa na zenye ubora unaohitajika.

Fauka ya hayo Dkt. Kiprono alisema mfumo huo pia utafanikisha utoaji maamuzi bora, uvumbuzi na ushirikiano mwafaka kati ya serikali ya taifa na zile za kaunti, pamoja na sekta ya kibinafsi, huku ukiwiainisha Kenya na viwango vinavyohitajika vya kimataifa kama vile malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).

Nguzo muhimu za mfumo wa KIAMIS ni muundo wa usimamizi, ambao unafafanua majukumu ya wizara ya kilimo na ustawi wa mifugo (MoALD), ikisaidiwa na serikali za kaunti na sekta ya kibinafsi.

Taasisi kuu zinazofanikisha mfumo huo ni pamoja na Baraza la usimamizi wa Takwimu  (DGC) na kamati ya kiufundi ya usimamizi wa takwimu, (DGTC), Kituo cha usimamizi wa ubora wa takwimu, Kinachotekeleza taratibu zifaazo kama vile kutoa maelezo na usawazishaji ili kuhakikisha ubora wa hali ya juu. Usalama wa takwimu na usiri: Inahakikisha ulinzi wa data dhidi ya wasioruhusiwa, miongoni mwa taasisi zingine.

Mfumo huo wa KIAMIS, unahakikisha takwimu zinafanikisha mipango dhabiti na utungaji wa sera, huku ukitekeleza jukumu muhimu la kufanyia merekebisho sekta ya kilimo kupitia uvumbuzi wa kidijitali.

Share This Article