Mfumo wa Kenya Power wa kununua tokeni za umeme wakumbwa na hitilafu

Martin Mwanje
1 Min Read

Kampuni ya Kenya Power, KP imetangaza kuwa mfumo wake wa kununua tokeni za umeme umekumbwa na hitilafu. 

Hii si mara ya kwanza kwa mfumo huo kukumbwa na hitilafu ya aina hiyo.

“Tunakumbana na hitilafu kwenye mfumo wetu wa kulipia umeme ambayo inaathiri ununuaji wa tokeni za umeme,” ilisema KP katika taarifa.

“Tunafanya kazi kurejesha hali ya kawaida haraka iwezekanavyo. Tunaomba radhi kutokana na usumbufu uliosababishwa na hali hiyo.”

Hitilafu hiyo imezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii huku Wakenya wengi wakielezea mahangaiko tele wanayokumbana nayo katika kununua tokeni za umeme.

Kunao waliopachika mitandaoni ujumbe waliopokea punde walipojaribu kulipia tokeni za umeme kwa njia ya M-Pesa.

“Mwamala wako ulishindikana, M-Pesa haiwezi ikakamilisha malipo yako kwa kampuni ya KPLC PREPAID. Mfumo wa kampuni hiyo wa kupokea malipo unakumbwa na changamoto fulani za kiufundi, jaribu wakati mwingine,” ulisema ujumbe kutoka kwa kampuni ya Safaricom.

Kwa sasa, nadhari ya Wakenya imeelekezwa kwa kampuni ya Kenya Power hususan kuhusiana na kasi itakayotumia kurejesha hali ya kawaida na kuwaepushia Wakenya usumbufu.

 

 

 

 

 

Share This Article