Mfalme Charles wa tatu wa Uingereza aliwasili nchini Jumatatu usiku akiwa ameandamana na mkewe Malkia Camilla.
Hii ndio ziara rasmi ya kwanza ya mfalme Charles wa tatu na Malkia Camilla katika taifa la Afrika na ya kwanza katika taifa la jumuiya ya madola tangu walipochukua hatamu, mwezi Mei mwaka 2023.
Mfalme huyo ambaye anafanya ziara rasmi ya siku nne nchini Kenya, aliwasili akiwa kwenye ndege ya jeshi la wanahewa la Uingereza muda mfupi kabla ya saa tano Jumatatu usiku.
Mfalme Charles anatarajiwa katika ikulu ya Nairobi leo Jumanne asubuhi kwa makaribisho rasmi kabla ya kushauriana na Rais William Ruto.
Makao ya Buckingham Palace yalisema kuwa mfalme Charles na Malkia Camilla watazuru maeneo kadha nchini.
Taarifa kutoka ubalozi wa Uingereza nchini ilieleza kuwa mfalme Charles na malkia Camilla watazuru mji wa Nairobi, kaunti ya Mombasa na maeneo mengine.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa ziara hiyo itadhihirisha ushirikiano ulioko baina ya mataifa haya katika kukabili athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kuzindua ajira kwa vijana, na kuboresha uhusiano ulioko baina ya ya Kenya na Uingereza pamoja na kudumisha usalama katika kanda hii ya afrika.
Ziara hii inajiri huku Kenya ikijitayarisha kwa maadhimisho ya miaka 60 tangu ijipatie uhuru na itazingatia kwa kina uhusiano mwema baina ya mataifa haya.