Mfalme Charles wa tatu wa Uingereza na Malkia Camilla, walizuru eneo la wanajeshi wa majini la Mtongwe Naval Base katika kaunti ya Mombasa, katika siku ya tatu ya ziara yao humu nchini.
Akiandamana na Rais William Ruto, mfalme huyo na malkia walishuhudia onyesho la kipekee la kutua ufuoni lililoandaliwa na wanajeshi wa majini wa Kenya na Uingereza chini ya wakufunzi wao wa British Royal Marines.
Hafla hiyo fupi ilikamilishwa na gwaride ya heshima iliyoandaliwa na jeshi la wanamaji nchini.
Wanajeshi wa majini wa Kenya walionyesha ujuzi wao kwa onyesho la kutua ufuoni katika ushirikiano wa kijeshi na mafunzo ya majuma 12 kutoka kwa wanajeshi wa Uingereza.
Kundi la kwanza la kikosi kipya cha Kenya Marine Commando, lilikamilisha mafunzo yake tarehe tano mwezi Mei mwaka huu.
Lengo kuu ni kugeuza kikosi hicho kuwa kikosi maalum cha vita ambacho kinaweza kutekeleza oparesheni mbalimbali ili kukabiliana na vitisho mbalimbali katika eneo hili.
Mkakati huo unalenga kubuni kitengo cha Kenya Marine Commando katika kipindi cha miaka mitano kwa usaidizi wa Marekani.
Ziara ya Mfalme Charles na Malkia Camila katika eneo la pwani imepiga jeki sekta ya utalii nchini.