Mfahamu Samora Machel

Dismas Otuke
5 Min Read

Alizaliwa tarehe 29, Sept. 1933 sehemu ya Chilembene iliyoko maili 200 kaskazini mwa mji mkuu – Maputo.

Alisomea shule ya Wamishonari.

Alikataa kuendelea na elimu ya juu ya dini na akajiunga na chuo cha ukunga mjini Maputo.

Kule hospitalini, ndiko alikoanza harakati za siasa kwa kupinga malipo duni waliyopewa wakunga Waafrika dhidi ya bora ya wazungu.

Alipohojiwa na mwanahabari kuhusu hilo, alisema kuwa “mbwa wa mzungu anapata chanjo bora na uangalizi mzuri wa matibabu kuliko mfanyakazi ambaye anajenga mali ya tajiri’’.

Baada ya kuhudumu kwa miaka 10, alijiunga na chama cha kisiasa cha Clandestine Mozambique Liberation Front (Frelimo), ambacho kilimtuma nchini Algeria kwa mafunzo ya kijeshi.

Aliporejea, aliongoza chama hicho katika vita dhidi ya ukoloni wa Ureno kwa muda mrefu na kumpelekea kupanda vyeo kwenye kikosi hicho.

Baada ya kifo cha kiongozi wao Eduardo Mondlane mwaka wa 1969, aliteuliwa kuwa kiongozi wa chama hicho mwaka wa 1970.

Mwaka wa 1975, kulitokea hali ya mapinduzi ya serikali nchini Ureno na hapo ndipo Mozambique ilipata uhuru naye Samora akawa rais.

Katika uongozi wake, alikuwa na misimamo mikali aliyoitaja kama iliyotokana na maisha ya wazazi wake waliolazimishwa kupanda mmea wa pamba kwa faida ya wakoloni na kisha wakafurushwa kutoka mashamba hayo kwa faida ya kuishi kwa wakoloni hao.

Alikubali chama kimoja na kukataa ukosoaji wa upinzani. Uongozi wake ulitaifisha taasisi zote, kujenga shule na hospitali.

Kabla ya uhuru wao, Samora alilipa kundi la Robert Mugabe (Rais wa kwanza wa Zimbabwe) makao ili lipambane na utawala wa mzungu mkoloni nchini Rhodesia (Zimbabwe) na Afrika Kusini.

Msumbiji ilipopata uhuru, mataifa hayo mawili yalilipiza kisasi kwa kubuni na kulifadhili kundi pinzani nchini Msumbiji – Mozambique National Resistance (Renamo) mwaka wa 1976, kwa lengo la kupinga Samora kuendelea kuunga mkono makundi yanayopinga serikali za wakoloni kusini mwa Afrika.

Kundi hilo liliua watu takriban 100,000, likaharibu reli, umeme, shule na hospitali na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa uchumi na wakimbizi zaidi ya millioni moja.

Hali hii iliisababisha Msumbiji kutegemea misaada hasa kutoka kwa umoja wa kisovyeti.

Zimbabwe ilipopata uhuru, kundi hilo lilibaki chini ya ufhadhili wa Afrika Kusini.

Maji yalipozidi unga, Samora alienda nchini Afrika Kusini mwaka wa 1984 na kutia saini mkataba wa ‘’Nkomati’’ uliopinga msaada kwa makundi pinzani ya mataifa mengine.

Hatua hiyo ilileta nafuu kati ya Frelimo na Frenamo ila baadhi ya maeneo yalishuhudia utovu wa usalama hivyo kumlazimu kutumia asilimia 40 ya Pato la Taifa (GDP) kwa usalama.

Mkataba huo pia ulikuwa wa kujenga uchumi wa mataifa husika ya kusini mwa Afrika.

Vile vile, utawala wake ulikumbwa na hali ngumu ya kiangazi na mafuriko.

Mwaka wa 1986 akiwa safarini kutoka nchini Zambia, ndege iliyombeba ilianguka usiku nchini Afrika Kusini na akafariki papo hapo pamoja wengine 33 huku tisa waliokuwa kwenye viti vya nyuma ya ndege wakinusurika.

Shutuma za kifo hicho zilielekezwa kwa serikali ya mbeberu wa Afrika Kusini ila walikanusha.

Alikuwa amepanga kufanya mabadiliko jeshini siku iliyofuata.

Kabla ya usafiri huo, taarifa za kijasusi kutoka kwa Wizara ya Usalama zilipendekeza kuwa asisafiri usiku.

Kifo chake kilisababisha maandamano jijini Harare.

Mkewe Graca Machel, baadaye aliolewa na rais wa kwanza wa Afrika Kusini Nelson Mandela na kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuolewa na marais wawili.

Akiwa huko, mwaka wa 1998, alitoa ushahidi kwa tume ya uwiano na maridhiano ya taifa hilo uliothibitisha kuwa serikali ya wakati huo ilihusika na kifo hicho.

Katika hali ya kumuenzi, amebakia kielelezo chema kwa mataifa mengi yanayopigana na ukoloni mamboleo.

Vile vile, sehemu ya ajali imetengwa kwa ukumbusho wake.

Jijini Harare, barabara kuu imeitwa jina lake sawia na mjini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Tunamkumbuka kwa kusema kuwa “mshikamano wa kimataifa si kitendo cha hisani: ni kitendo cha umoja kati ya washirika wanaopigana kwa ardhi tofauti kwa lengo moja. Mwanzo wa hayo malengo ni kufanikisha maendeleo ya binadamu kwa viwango vya juu’’.

TAGGED:
Share This Article