Mshambuliaji wa Argentina na Inter Miami Lionel Messi amechaguliwa kuwa Mwanariadha Bora wa Mwaka wa jarida la Time.
Messi alijiunga na Miami mnamo mwezi Julai na kufunga mabao 11 katika michezo 14 kwenye mashindano yote na kuwasaidia kubeba Kombe la Ligi, taji lao la kwanza kabisa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 pia alishinda Ballon d’Or kwa mara ya nane mwezi Oktoba.
“Lionel Messi mwaka huu alifanikiwa kufanya kile ambacho kilionekana kutowezekana, wakati aliposajiliwa na Inter Miami: kuigeuza Marekani kuwa nchi ya soka,” Jarida la Time limeandika.
Jarida hilo lilisema kuwasili kwa Messi kumesababisha kuongezeka kwa mashabiki, bei za tiketi, mauzo ya bidhaa na watazamaji wa michezo ya MLS.
Mshambuliaji huyo anaungana na mchezaji wa mazoezi ya viungo Simone Biles, muogeleaji Michael Phelps na nyota wa NBA LeBron James kushinda tuzo hiyo.
Baada ya kuondoka Paris St-Germain mwishoni mwa kandarasi yake, Messi alisema upendeleo wake ulikuwa kurejea kwa kihisia katika klabu ya utotoni ya Barcelona, lakini uhamisho huo haukutimia.
Baadaye, chaguo likawa kwenda Miami au kuhamia Saudi Pro League, ambayo imewekeza zaidi katika talanta za kigeni misimu miwili iliyopita.
“Chaguo langu la kwanza lilikuwa kurejea Barcelona, lakini haikuwezekana. Nilijaribu kurudi, na haikufanyika,” aliambia Time.
“Ni kweli pia kwamba baadaye nilikuwa nafikiria sana kwenda kwenye ligi ya Saudia, ambako naifahamu nchi hiyo na wametengeneza ushindani mkubwa ambao unaweza kuwa ligi muhimu katika siku za usoni. Ilikuwa Saudi Arabia au MLS, na chaguzi zote mbili zilionekana kuvutia sana kwangu.”