Mercy Chinwo afunguka kuhusu utata kati yake na meneja wake wa zamani

Meneja huyo kwa jina Eezee Tee alikuwa amedai kwamba Chinwo na Judi Kay walimshtaki mahakamani madai ambayo Mercy amekanusha akisema yalilenga kuwaharibia sifa

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Nigeria Mercy Chinwo amezungumza kuhusu utata uliopo kati yake na aliyekuwa meneja wake kwa jina Ezekiel Onyedikachukwu maarufu kama Eezee Tee.

Katika video aliyochapisha kwenye akaunti yake ya Instagram, Chinwo alisema kwamba Eezee Tee amemnyanyasa, ametishia maisha yake na amehusika pakubwa katika uvumi unaosambazwa kuhusu baba halisi wa mtoto wake.

Chinwo ambaye alikuwa amejawa na hasira kiasi cha kulia akijieleza alisema kwamba Eezee Tee alimtishia sana akalazimika kuhama kutoka Lagos hadi Port Harcourt.

Mwimbaji huyo alikanusha madai ya kwamba alimshtaki meneja huyo wa zamani mahakamani akiongeza kusema kwamba aliahidi kumharibu kabisa kwa sababu yeye ndiye alimkuza kama mwimbaji.

“Nimevumilia maonevu, nimevumilia vitisho, chochote kinachoendelea mitandaoni ni kidogo ikilinganishwa na yale ambayo nilipitia.” alisema Mercy huku akitiririkwa na machozi.

Kosa lake kubwa anasema ni kushirikiana kurekodi wimbo na mhubiri Nathaniel Bassey ambaye kulingana naye Eezee Tee hampendi ndiposa akaanzisha uvumi kwamba Bassey ndiye baba ya mtoto wake.

Alifafanua kwamba Eezee alijaribu kumlazimisha atie saini makubaliano ya miaka 12 akakataa na hivyo akanyimwa mirahaba ya nyimbo zake kwa muda wa miaka miwili.

“Baada ya mkataba wangu kufikia kikomo niligundua kwamba umegushi mkataba mwingine . Ambia ulimwengu kilichofanyikia mikataba ya mwaka 2017 na 2019” alisema mwimbaji huyo akimlenga Eezee.

Awali Eezee Tee alikuwa amedai kwamba Chinwo na Judi Kay walikuwa wamemshtaki mahakamani madai ambayo Mercy amekanusha akisema yalilenga kuwaharibia sifa.

Share This Article